TANZANIA

Halmashauri za Tanzania Zaagizwa Kutenga na Kutoa Fedha za Lishe - Mhe. Ndejembi

SEPTEMBA 27, 2023
Border
news image

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali nchini Tanzania Mhe.Deogratus Ndejembi amezitaka Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kutenga fedha na kutoa kiasi cha sh.1000 kama Serikali ilivyowaelekeza ili kutokomeza madhara yatokanayo na lishe duni kwa maendeleo ya Taifa.

Mhe.Ndejembi amesema hayo Mkoani Dodoma wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri Nchi, Ofisi ya Rais TAMASEMI. Mhe. Mohamed Mchengerwa katika uzinduzi wa Kitabu cha Kumbukumbu za sauti za Walengwa wa Mradi wa USAID Lishe Endelevu na Kufunga Mradi kwa Ngazi ya Taifa.

Amesema Tanzania imeweza kupiga hatua kubwa katika kudhibiti utapiamlo na ushirikishwaji wa wadau wa sekta zote ambao vipaumbele vyao vinachangia kuboresha hali ya Lishe na Afya ya Jamii nchini umekuwa ni nguzo ya mafanikio kwa nchi na uboroeshaji wa lishe ya jamii yetu ni suala mtambuka linalohitaji kila mtu, kila sekta na kila mdau ashiriki kikamilifu.

“Ninamshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluh Hassan kwa msukumo mkubwa aliouweka katika suala la kuwekeza katika lishe na hususan siku elfu moja za mwanzao za maisha ya mtoto ambapo siku 1000 zinapatikana kuanzia siku mimba inapotungwa hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka miwili. Amesema Mhe. Ndejembi

Amesema Tanzania imepiga hatua katika kutokomeza udumavu matokeo ya utafiti wa Kitaifa(Tanzania National Demographic Health Survey -TDHS) wa mwaka 2015/16 ilionesha udumavu ulikuwa 34% na mwaka 2022 udumavu umeshuka kufika 30%.

“ukiangalia Mkoa wa Dodoma na Rukwa ambapo Mradi wa Lishe Endelevu umetekelzwa kumekuwa na punguzo la udumavu kwa wastani wa 6% na 6.5.”

Mhe. Ndejembi

Ameziagiza Halmashauri kuendelea kutenga na kutoa fedha sh.1000 kwa kila mtoto chini ya miaka mitano kwa 100% au zaidi kwa ajili utekelezwaji wa afua za lishe, kusimamia kikamilifu utekelezaji wa masuala ya lishe kama yalivyoanishwa katika mpango jumuishi wa lishe wa mwaka 2021/22 mpaka 2025/26 na hususan afua zote za lishe zilizokuwa zinasimaiwa na mdau ziingizwe katika mpango kabambe wa Halmashauri.

Pia amewataka viongozi wa Kata,Vijiji na Mitaa kuwajibika na kuhakiakisha wanawasimamia ipasavyo watendaji walio katika maeneo yao kusudi swala la lishe liendelee kupewa kipaumbele katika maeneo yote na kuzitaka Halmashauri kuhakikisha zina motisha kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwani wao ndio nguzo kubwa ya utekelezaji wa afua za lishe.

Kwa upande wa Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulika Afya Dkt. Charles Mahera amesema suala la lishe watanzania wanatakiwa kulipa kipaumbele sababu lishe bora husababisha kuwa na afya bora na wananchi bora katika masuala mbalimbali kwa sababu lishe inasaidia ukuaji wa akili.

Naye Mkurugenzi Mkazi Save The Childrean Bi. Angela Kauleni amesema, udumavu kwa watoto una madhara makubwa ambapo ni pamoja na kuathirika kwa makuzi, ukuaji na kupevuka kiakili, kimwili na kisaikolojia kwa watoto pia watoto wenye udumavu wako kwenye hatari ya kutofikia uwezo wao katika makuzi, elimu na usatwi wao wao kiuchumi na hivyo kuathiri Taifa kwa kukosa kizazi chenye tija.

Ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo na kuiomba kuipa agenda ya lishe kipaumbele.

Mradi wa USAID Lishe Endelevu kwa kushirikiana na Serikali na Watu wa Marekani ulitekelezwa ulianza mwaka 2019 na kutekekezwa katika Mkoa wa Rukwa, Dodoma,Morogoro na Iringa.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania