Serikali ya Tanzania imesema changamoto ya malezi na makuzi ndiyo sababu kubwa inayochangia watu kujinyonga kwa kukosa ustahimilivu na mbinu sahihi za kukabiliana na changamoto ya maisha.
Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wanawake na Makundi Maalum alipokuwa amemuwakilisha Waziri wa wizara hiyo Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kuzuia Kujiua Duniani yaliyofanyika katika Hospitali ya Taifa ya Akili (Mirembe) Jijini Dodoma.
“Serikali imejipanga kuhudumia wananchi kupambana na changamoto ya tatizo la afya ya akili kwa kutoa elimu na kuja na ainisha afua zakuzuia wananchi kujiua kwani kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) watu kiasi cha laki saba hujinyonga duniani kwa mwezi mmoja,” ameeleza Wakili Mpanju.
Aidha Wakili Mpanju ameeleza kuwa wimbi kubwa la wahanga wa kujiua ni watoto na vijana ambao wamekosa misingi sahihi ya kukabiliana na maisha ikiwemo pia jamii kukosa hofu ya Mungu .
“Utu wa mtu una thamani, changamoto za maisha zinapita, na kujiua si suluhu ya maisha, watu wasijitenge na kuwa upweke, wafike sehemu sahihi ili waweze kupata msaada wa kisaikolojia.” Amehimiza Wakili Mpanju.
Kwa upande wake daktari wa Afya ya akili Mirembe Dkt. Innocent Mwombeki, amebainisha kwamba idadi ya watu wenye changamoto ya akili inaongezeka kwani kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, utafiti unabainisha kuwa watu 3000 hujiua kwa siku moja.
“Katika kukabiliana na kutatua janga la kujiua, nchi nyingi duniani zimeondoa kosa la kujinyonga kwenye makosa ya jinai kwani tatizo hili linahusiana zaidi na hali ya akili ya mtu ambapo wanaokutwa wakitaka kujiua wanakua na changamoto za kiakili, ” amesema Dkt Mwombeki.
Naye Mwakilishi wa Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mhe. Godwin Gondwe amesema hali ya janga la akili bado ni changamoto mkoani humo kwani tafiti zinaonyesha kuwa watu 10 kati ya 99 hubainika kutaka kujiua kwa siku moja.
“Serikali inapambana kuhakikisha tunaondokana na janga hili hivyo natoa rai kwa wadau mbalimbali kuhakikisha kwamba tunaipunguza changamoto hii kwani Serikali peke yake haiwezi kukalibiana nayo peke yake, ” amesema Mhe. Gondwe.