TANZANIA

Fedha Za Wadau Wa Maendeleo Zitumike Kutatua Changamoto Za Wananchi

SEPTEMBA 22, 2023
Border
news image

Watalamu wa Afya nchini wametakiwa kuwa wazalendo katika kusimamia fedha zinazotolewa na wadau wa maendeleo, ili kuhakikisha wanatatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi kama ilivyo azma ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Wito huo umetolewa Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel wakati akifunga kikao kazi cha tathmini ya namna Tanzania ilivyoweza kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19.

Dkt. Mollel amesema kuwa wadau wengi wamekuwa wakileta fedha nyingi kwenye sekta ya afya, lakini fedha hizo zimekuwa hazitumiki ipasavyo katika kusaidia sekta hiyo, huku nyingine zikiishia kutumika katika semina na makongamano na kupelekea kushindwa kuwanufaisha wananchi ambao ndiyo walengwa.

“Zinakuja fedha nyingi kutoka kwa wadau, lakini tukishuka chini katika ngazi ya msingi hatuoni matokeo chanya, tuige mfano wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan namna alivyotumia fedha za COVID katika kuboresha huduma za afya nchini mfano katika ngazi ya msingi kumejengwa majengo ya dharura na majengo ya wagonjwa mahututi.” Amesisitiza Dkt. Mollel.

Akizungumzia kuhusu zoezi la tathmini baada ya kukabiliana na mlipuko wa UVIKO-19 Dkt. Mollel amesema yapo mengi ya kuzungumzia katika tathmini hiyo, hivyo ni jukumu la wataalamu na wadau walioshiriki kwenye kikao hicho kuhakikisha tathimini yao inakuja na matokeo chanya ya kuleta tija kwa wananchi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa Wizara ya Afya, Dkt. Angela Samwel amesema mapendekezo yote yaliyotolewa na watalaamu pamoja na wadau walioshiriki kwenye tathmini hiyo yatachukuliwa kama sehemu ya kupokea masuala yote mazuri na kuboresha mapungufu yaliyojitokeza wakati wa kukabiliana na mlipuko wa UVIKO-19.

Dkt. Angela ameongeza kuwa Tathmini ya namna nchi ilivyokabiliana na mlipuko wa UVIKO 19 imehusisha wadau mbalimbali kutoka Wizara mbalimbali ikiwemo, Taasisi za Serikali, Hospital za Taifa, Hospital binafsi, Waganga wakuu wa mikoa,wadau wengine kutoka Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Wadau wengine wa Maendeleo.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania