TANZANIA

Dkt. Tulia Kuwasomesha Watoto Yatima Mbeya, Achangia Ujenzi wa Nyumba

SEPTEMBA 9, 2023
Border
news image

Spika wa Bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ameahidi kuwasomesha watoto watano yatima ambao wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu.

Watoto hao wanaoishi katika Kata ya Hanseshelo iliyopo Jijini Mbeya wapo katika mazingira magumu baada ya wazazi wao kufariki ambapo baba yao aliuawa na watu wasiojulikana miezi kadhaa iliyopita

Dkt. Tulia ametoa ahadi hiyo leo tarehe 9 Septemba, 2023 wakati wa hafla ya kukabidhi nyumba kwa familia hiyo iliyojengwa kwa michango ya wasamaria wema na kusimamiwa na Kanisa la KKKT Usharika wa Uyole ambapo amechangia Shilingi Milioni 2 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo.

Dkt. Tulia amewataka Wananchi kuendeleza desturi ya kusaidiana katika jamii zao ikiwemo pale wanapoona kuna wenzao hususani watoto wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi ili kuwezesha kujenga kizazi bora hapo mbeleni.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania