TANZANIA

Dkt. Biteko Ameiagiza Wizara ya Ardhi Nchini Tanzania Kupima na Kupanga Ardhi kwa Ufanisi

SEPTEMBA 9, 2023
Border
news image

Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Doto Biteko amezindua Kituo cha Taifa cha ubunifu na mafunzo ya teknolojia ya taarifa za kijiografia na kuagiza kitumike kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwa chachu katika sekta ya ardhi.

“Itakuwa bahati mbaya sana watu wageuze kujifunza hapa kwa ajili ya kulipwa posho ya mafunzo, kiwe kituo ambacho kitaongeza thamani na Mheshimiwa Waziri wizara yako ni moyo wa shughuli zote za uchumi hapa nchini, inahitaji msukumo mkubwa sekta yako ya ardhi,nikutie moyo waziri na watendaji wengine pamoja na kazi kubwa iliyofanyika ya kuimarisha sekta hii na amini na watanzania ni mashahidi bado tuna kazi ya kufanya,”amesema Dkt. Doto Biteko.

Amehimiza mipango ya Halmashauri iendane na Wizara ili kukidhi matarajio ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya ardhi, “Wataalam wako wa ardhi imarisheni ushirikiano pamoja na halmashauri, haina maana yoyote huku wizarani unapanga mambo yako na halmashauri inapanga mambo yake mkija kuanza kutekeleza unakuta wizara inachosema na halmashauri havikutani mahali popote,” amesema Naibu Waziri Mkuu.

Naye, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry Silaa amesema Serikali ya Tanzania Kwa kushirikiana na Serikali ya Korea imechukua hatua za kukabiliana na changamoto za ardhi kwa kuanzisha kituo hicho.

Amesema Wizara hiyo ina changamoto ya ukosefu wa teknolojia za kisasa katika upatikanaji wa taarifa za kijiografia na mifumo ya usimamizi wa ardhi na kupelekea kupungua kwa kasi ya upangaji , upimaji,uthamini na umilikishaji ardhi hivyo kituo hicho kinatarajiwa kumaliza kero zote.

"Serikali yetu imeweka historia leo ya kuweka alama mbili muhimu ambayo ni kuzindua kituo cha kitaifa Cha Ubunifu na mafunzo ya taarifa za kijiografia na kuwatunuku vyeti wahitimu 11 waliopata mafunzo ya kurusha ndege zisizo na rubani tatu. ukusanyaji wa taarifa za kijiografia na uchakataji wa taarifa za kijiografia".

Silaa ametumia nafasi hiyo kuwataka viongozi wa kituo hicho kujipanga na kuwa na maono ya kukiendeleza kituo ili kiwe Taasisi pekee ya ubunifu na usimamizi wa taarifa za kijiografia nchini na kwamba Wizara itaendelea kutoa ushauri na kukilea kituo hicho ili kifikie malengo yake na kusaidia kutatua changamoto ya wataalam wenye weledi na ujuzi wa teknolojia ya kisasa ya usimamizi taarifa za kijiografia,"amesisitiza

Naye, Balozi wa Korea nchini Tanzania Kim Sun Pyo, amesema kuzinduliwa kwa kituo hicho ni manufaa kwa wananchi wa Dodoma kwakuwa wataweza kunufaika hasa katika suala zima la upimaji wa ardhi ambao sasa unakwenda kufanyika kwa ubora na kwa bei nafuu.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga ameeleza kuwa kituo hicho kina lengo la kujengea uwezo watumishi na wadau kukidhi mahitaji ya teknolojia ya kisasa ya usimamizi wa taarifa za kijiografia nchini kwa kutoa mafunzo yenye ujuzi maalum na kwamba itasaidia kusambaza na kubadilishana taarifa Kwa manufaa ya watanzania.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania