TANZANIA

Dkt. Msonde Awapa Somo Walimu Kuongeza Umahiri Wa Lugha Ya Kingereza Sekondari Tanzania

OKTOBA 02, 2023
Border
news image

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini Tanzania Dkt. Charles Msonde amewataka walimu kuongeza umahiri wa kuongea na kuandika lugha ya kiingereza kwa wanafunzi wa sekondari.

Akifungua mafunzo kwa wakuu wa shule za Sekondari kuhusu ufundishaji wa awali wa Kingereza kwa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba kwa Mkoa wa Dodoma, yaliyofanyika Chuo Cha Ualimu Mpwapwa, Dkt.Msonde amesema ni vyema kubainisha tatizo na kutafuta njia mbadala ya kuwawezesha watoto kujua lugha ya kiingereza.

Amesema mwalimu anawajibu wa kufundisha wanafunzi umahiri wa kuandika na kuongea kingereza.

"Mahali popote penye changamoto lazima itatuliwe ila kinachotakiwa ni kutambua nguvu na shida ipo wapi hivyo ukiweza kuipata changamoto na kuweza kuitatua unaleta mabadiliko,"amesema.

Amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Dodoma kwa kuamua kwa dhati kushirikisha Halmashauri zao kwa kuhakikisha wanatafakari kwa kina changamoto zinazoikabili sekta ya elimu nchini hasa katika kipindi hiki ambacho serikali ina makakati wa kuboresha elimu nchini.

"Serikali imeamua kuleta mabadiliko katika English Orientation Course kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi waliomaliza darasa la saba wanajua kuandika, kusoma na kuongea kingereza lengo ni mwalimu aweze kueleweka pale anapofundisha darasani,"amesema.

Amesema kuwa lugha ndio msingi wa kila kitu na hasa kwa shule za sekondari hivyo amewataka Wakuu wa shule kuhakikisha wanatatua changamoto hiyo shuleni.

“Katika kuhakikisha unatatua changamoto wa kitu fulani lazima utambue nguvu ya adui hivyo tunapotaka kuboresha elimu ya sekondari tutambue changamoto kubwa ya wanafunzi wa sekondari ni umahiri wa lugha ya kingereza hivyo ni vyema kubainisha tatizo na kutafuta njia mbadala ya kuwawezesha watoto kujua lugha ya kiingereza,"amesema.

Naye, Afisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, Gift Kyando amesema dhamana ya elimu kwa upande wa shule za sekondari ipo mikononi kwa Walimu Wakuu wa shule hivyo wanawajibu wa kuwafundisha watoto umahiri wa kujua na kutambua lugha ya kingereza nchini.

Amesema kuwa Mkoa wa Dodoma inatarajia kuanza Orientation kwa kidato cha kwanza kuanzia Oktoba 9, 2023 hivyo imeamua kuwajengea uwezo walimu ili waweze kutimiza lengo la Mkoa la kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania