TANZANIA

Dk. Mpango Asisitiza Serikali Kushirikiana na Madhehebu Mbalimbali

OKTOBA 06, 2023
Border
news image

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema serikali itaendelea kufanya kazi na kushirikiana vema na Kanisa Katoliki pamoja na madhehebu mengine ya dini hapa nchini.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa mapokezi ya Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa yaliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam akitokea Vatican alipopewa hadhi ya Ukardinali. Amempongeza Kardinali Rugambwa kwa kuendelea kuhubiri amani na umoja wa Watanzania na kumsihi kuendelea kuwa chachu ya amani, upendo na umoja. Makamu wa Rais amesema ni baraka kwa Taifa la Tanzania kupata Kardinali wa tatu.

Kwa upande wake Mwadhama Kardinali Protase Rugambwa amewaomba watanzania wa kila dini kuendelea kumuombea ili aweze kufanya vema kazi hiyo kwa uaminifu na kuweza kuleta maendeleo ya mwanadamu kwa ujumla kuanzia hapa nchini kimwili na kiroho na baadaye hata nje ya nchi.

Kardinali Rugambwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Kanisa, Serikali na watanzania wote waliomtia moyo na kumtumia jumbe mbalimbali za pongezi zilizompa moyo na kumuimarisha.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania