TANZANIA

Daraja La Mawe La Ngano Mkombozi Kwa Wananchi Wa Iringa Tanzania

OKTOBA 03, 2023
Border
news image

Wananchi wa Vijiji vya Ngano, Igula , Ilambilole na Mikongwi vilivyopo Kata ya Kihorogota katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa nchini Tanzania wameishukuru Serikali kwa kuwajengea Daraja la mawe la Ngano lenye urefu wa mita 34 linalounganisha vijiji hivyo pamoja na vijiji vingine vya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.

Wakiongea kwa nyakati tofauti, wananchi hao wameeleza kuwa hapo awali walikuwa hawawezi kusafiri na kusafirisha mazao yao kwa urahisi hasa kipindi cha masika kutokana na kukosekana kwa kivuko.

Bi. Imelda Kipunga, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Maganga alisema kuwa watu wengi walipoteza maisha hasa kipindi cha masika kutokana na maji mengi kujaa na watu kushindwa kuvuka kutokana na kukosekana kwa daraja, hivyo wanaishukuru Serikali kwa kuwajengea daraja hilo ambapo kwasasa wanaweza kusafiri na kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi.

“Eneo hili lilikuwa halipitiki kutokana na korongo lililokuwepo kabla ya daraja, watu wengi walipoteza maisha wakijaribu kuvuka korongo hili ambalo wakati wa mvua maji mengi yalikuwa yanajaa, tunashukuru Serikali kwani wakati wa ujenzi wa daraja watu wetu walipata ajira kutokana na kusomba mawe yaliyotumika kujengea daraja hili”, alisema Bi. Imelda.

Naye Bw. Ezekiel Amos, Mkazi wa kijiji cha Igula ameishukuru Serikali kupitia TARURA kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo limewasaidia kusafirisha mazao yao kutoka mashambani kwenda sokoni na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.

Kwaupande wake Meneja wa TARURA Wilaya ya Iringa, Mhandisi Barnabas Jabir alieleza kuwa lengo la Wakala katika Wilaya hiyo ni kuhakikisha wananchi wanasafiri na kusafirisha mazao yao ikiwa ni utekelezaji wa mpango mkakati wa pili wa Wakala wa kufungua Barabara ili kuwezesha wananchi kufika kusiko fikika.

“Tumejenga daraja hili kwa kutumia teknolojia ya mawe ambapo daraja hili lina urefu wa mita 34 na limegharimu shilingi milioni 225, mradi umekamilika kwa wakati na wananchi wanazifikia huduma za kijamii kwa urahisi”, alisema Mhandisi

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inatarajia kutumia takribani shilingi Bilioni 4.7 Katika Wilaya ya Iringa ili kufungua barabara, kufanya matengenezo ya Barabara kwa lengo la kuwezesha wananchi kusafiri kwa urahisi, kusafirisha mazao kwenda sokoni na kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania