TANZANIA

Bilioni 7.3 Kutumika Kukabiliana Na Madiliko Ya Tabia Nchi Tanzania

SEPTEMBA 8, 2023
Border
news image

Serikali ya Tanzania imenufaika na shilingi bilioni 7.3 kutoka Serikali ya Norway kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na inayotekelezwa nchini

Hayo yamejiri baada ya Serikali hizo mbili kusaini Makubaliano ya kushirikiana katika shughuli za mazingira, hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Tanzania itajengewa uwezo katika utekelezaji wa shughuli za mazingira

Alisema makubaliano hayo ni chachu katika kuijengea Tanzania kuweza kunuifaika na fedha za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kutoka nchi zilizoendelea ambazo ziliahidi

Pia, alisema Norway imeiunga mkono Tanzania katika mikakati yake ikiwemo kupunguza gesi joto, utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira wa mwaka 2022 hadi 2032 pamoja Sera ya Uchumi wa Bluu.

“Makubaliano tuliyosaini leo yatasaidia katika miradi yetu ya kimazingira katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, nishati, maji, afya na ardhi na tuishukuru sana Serikali ya Norway, na sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais tunafurahi sana kwa miradi hii ambayo inakwenda kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” alisema Dkt. Jafo

Kwa upande wake Waziri anayeshughulikia masuala ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa na nchi za Nordic Mhe. Anne Beathe Tvinnereim aliyesaini kwa niaba ya Serikali ya Norway alisema kuwa makubaliano hayo ni matunda ya uhusiano wa muda mrefu wa Serikali hizo mbili

Alisema nchi yake imejipanga katika kuyatendea haki makubaliano hayo kwa kuelekeza miradi hiyo kwa wananchi wanaokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo yao

Mhe. Anne alisema kuwa Serikali ya Norway kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kufanya utafiti kwa ajili ya katika kuimarisha usimamizi wa Biashara ya Kaboni ambayo imeshika kasi hapa nchini.

Naye Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji na Maendeleo (UNFCC) Bw. Peter Malika alisema fedha hizo zilizotolewa zitasambazwa katika wilaya sita za Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kusaidai katika miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi

Alisema pia kutakuwa na mafunzo kwa jamii zilizoathirika na mabadiliko ya tabianchi kuhusu namna ya kutambua changamoto hizo kwa ajili ya mikakati ya kuanzisha miradi.

Aprili 21, 2008 nchi hizo mbili zilisaini makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi hatua iliyoanzisha Kituo cha Taifa Kufuatilia Kaboni (NCMC)

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania