TANZANIA

Bilioni 268 Zimeelekezwa Mtwara Tanzania Kwenye Barabara, Kuufungua Mkoa Wa Mtwara Kiuchumi

SEPTEMBA 16, 2023
Border
news image

Waziri wa Ujenzi nchini Tanzania Mhe. Innocent Bashungwa amesema shilingi Bilioni 268 zimetengwa kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Mtwara - Newala Masasi (km 210) sehemu ya Mnivata - Newala - Masasi (km 160) kwa kiwango cha lami ili kuufungua mkoa wa Mtwara kiuchumi, kijamii na kuchochea biashara katika ukanda huo wa Mikoa ya Kusini mwa Tanzania.

Ameeleza kuwa ukamilishaji wa mradi huo kwa ujumla utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 361 na miradi hiyo itatekelezwa kwa muda wa miezi 36.

Waziri Bashungwa ameeleza hayo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliofanyika katika uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Waziri Bashungwa ameeleza kuwa mpaka sasa Sehemu ya barabara ya Mnivata – Mitesa (km 100), Mkandarasi amekwishakabidhiwa eneo la mradi kwa ajili ya kuanza utekelezaji na Sehemu ya Mitesa – Masasi (km 60) pamoja na Ujenzi wa Daraja la Mwiti taratibu za kumpata mkandarasi ziko katika hatua za mwisho.

Aidha, Ameeleza kuwa Wizara inaendelea na juhudi za kuunganisha sehemu mbalimbali za mikoa ya nchi yetu na nchi jirani kwa barabara za lami zikiwemo nchi za Msumbiji, Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya.

"Baadhi ya barabara zilizokwishakamilishwa kwa kiwango cha lami na kuunganisha nchi yetu nchi jirani ni Mtwara – Lindi (Mingoyo) – Masasi – Tunduru – Ruvuma hadi Mbambabay; Songea – Makambako; na barabara ya TANZAM highway", amefafanua Waziri Bashungwa.

Bashungwa amemuahidi Mhe. Rais kuwa Wizara yake itakuwa ya vitendo na katika kauli mbiu ya Kazi Iendelee kazi inakwenda vizuri sana ambapo kwa sasa barabara za Mijini na Vijijini zinaendelea kutekelezwa kasi.

"Mhe. Rais Sekta ya Ujenzi ni ya Vitendo na kwa kuhakikisha mambo yanaenda nimeelekeza TANROADS kuimarisha mashirikiano na TARURA ili kuboresha mawasiliano ya Barabara Mijini na Vijijini kwa kasi zaidi kama ILANI ya CCM inavyotuelekeza", amesisitiza Bashungwa.

Ametaja miradi mingine ya barabara inayoendelea mkoani humo ikiwemo barabara ya Masasi – Nachingwea – Liwale (km 175) kwa Kiwango cha Lami kwa utaratibu wa Engineering, Procurement, Construction and Financing (EPC+F) ambao mkataba wake ulisainiwa tarehe 16 Juni 2023 kati ya TANROADS na Mkandarasi M/S China Railway 15 Bureau Group Co. Ltd.

Kadhalika, Waziri Bashungwa amemuhakikishia Mhe. Rais kuwa Wizara itahakikisha Taasisi za Kikandarasi na Kihandisi zilizo chini yake, zinatumika vizuri katika kufuatilia utekelezaji wa Miradi ya Ujenzi nchini, na kuhakikisha kazi zinakamilika kwa viwango vinavyokubalika kimikataba, kwa muda uliopangwa, ili Wananchi wapate huduma iliyokusudiwa kwa wakati.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania