TANZANIA

Bendera ya Tanzania Imepeperushwa Vyema Katika Mashindano ya FEASSSA Nchini Rwanda: Dkt. Msonde

AGOSTI 28, 2023
Border
news image

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI (Elimu), nchini Tanzania Dkt. Charles Msonde amezipongeza Timu za Wanafunzi wa Tanzania kwa kupeperusha vyema Bendera ya Taifa katika Mashindano ya michezo ya shule za Msingi na Sekondari wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSSA) yanayofanyika nchini Rwanda.

Dkt. Msonde ameeleza hayo leo tarehe 28 Agosti 2023 katika Ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda wakati Timu ya Wanafunzi, Walimu na Viongozi walipotembelea Ubalozi huo katika Mji wa Kigali pindi wakiwa safarini Kulejea nchini

“Vijana wetu wamepigania Taifa lao kwa kuubeba Utanzania na Wamelinda heshima ya Tanzania katika Mashindano haya ya Shule katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki” Amesema Dkt. Msonde

Akitoa taarifa katika Ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda, Dkt. Msonde ameeleza kuwa Tanzania imetwaa ubingwa na makombe katika michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Makombe manne katika mchezo wa goli kwa wanafunzi wa msingi na Sekondari.

Aidha, Dkt. Msonde amesema Tanzania imetwaa Ubingwa katika mchezo wa Wavu (Wasichana) wa shule za msingi, pia Tanzania imeshika nafasi ya pili katika michezo ya Soka, Netiboli na Tennis.

Katika Mashindano ya riadha, amesema Tanzania imetwaa medali 20 katika mbio zenye umbali tofauti tofauti kwa wanafunzi wa sekondari na msingi kwa wavulana na Wasichana.

Kadhalika, Dkt. Msonde ameushukuru Ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda kwa kuonyesha ushirikiano mkubwa kwa kipindi ambacho timu zilingia nchini katika Mashindano yaliyoanza tarehe 17 Agosti 2023.

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Bi. Happiness Rwehangisa amewapongeza na kuwashukuru Wanafunzi hao kwa kuonesha nidhamu, heshima na maadili ya Kitanzania kwa kipindi chote walichokuwa nchini Rwanda.

Oliver G Nyeriga - MTV Tanzania