TANZANIA

DHAMIRA YA RAIS SAMIA NI KUHAKIKISHA KILA MWANANCHI ANANUFAIKA NA UTALII WA ARUSHA- RC MAKONDA

Aprili 30, 2024
Border
news image

Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amesema dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa Kila mwananchi wa Arusha ananufaika na sekta ya Utalii.

Leo Aprili 30, 2024 wakati wa Kongamano la uwekezaji kwenye sekta ya Utalii mkoani Arusha, Mhe. Makonda amewaambia washiriki wa kongamano hilo kuwa zipo pia jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali yake ili kuweka mazingira mazuri ya wananchi kuweza kunufaika na fursa ya Utalii mkoani Arusha.

Mkuu wa Mkoa amesema serikali yake ya Mkoa imewekeza nguvu kubwa zaidi katika suala la Ulinzi na usalama ili kuhakikisha wageni na watalii wanaifurahia Arusha na kutoa fursa kwa wawekezaji na wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa uhuru zaidi.

Akizitaja hatua ambazo amezichukua katika kutimiza maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza Utalii Mkoani Arusha, Mhe. Makonda amesema tayari serikali ya Mkoa imeanza kufunga Kamera za ulinzi na taa za barabarani kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa na hadi kufikia mwezi wa saba mwaka huu, Mkoa wa Arusha anataka uwe mkoa unaoongoza kwa kuwa na kamera na Taa nyingi kuliko mkoa mwingine wa Tanzania.

Mhe. Mkuu wa mkoa ametumia fursa hiyo pia kuiomba serikali kufanya Marekebisho ya barabara za mkoani Arusha kutokana na ubovu mkubwa kwenye barabara za katikati ya Jiji na barabara za kuingia kwenye Mbuga na hifadhi zilizopo pembezoni mwa mkoa wa Arusha.

Aidha Mkuu wa Mkoa pia amesema tayari wameanza mchakato wa kutumia Jeshi la Kujenga Taifa JKT ili kusaidia katika usafi wa Jiji la Arusha kutokana na mitaa yake mingi kukithiri kwa uchafu na mitaro kujaa takataka.

Mhe. Mkuu wa Mkoa amesisitiza suala la matumizi ya teknolojia na uchache wa taasisi za udhibiti Mkoani Arusha kwa kuhimiza kuwa na kituo kimoja cha huduma za udhibiti ili kupunguza muda wa kumuhudumia muwekezaji anayetaka huduma za serikali wakati wa uwekezaji wake,akisema tamanio lake ni kuhakikisha Muwekezaji anatumia siku moja tu ili kupata huduma kwenye taasisi zote za serikali.

Mhe. Mkuu wa Mkoa kadhalika ametumia nafasi hiyo kuomba wananchi kujitokeza kwa wingi Leo jioni kwenye mkesha wa kuamkia maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani yanayotarajiwa kufanyika Mjini Arusha kwenye Uwanja wa Michezo wa Sheikh Amri Abeid, maadhimisho yatakayoongozwa na Rais wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

MTV Tanzania